Jumanne 2 Desemba 2025 - 13:50
Kwa Nini Safari ya Kamanda wa Jeshi la Lebanon Kuelekea Marekani Ilifutwa?

Hawza/ Gazeti la “An-Nahar” liliripoti kuwa moja ya sababu za kufutwa kwa safari ya Kamanda wa Jeshi la Lebanon kwenda Marekani ilikuwa ni kupinga kwake kushiriki mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika pamoja na maafisa kadhaa wa juu na maafisa wa kijeshi waliounganishwa na balozi, wakiwemo pia maafisa kadhaa wa “Kizayuni”.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, gazeti la “An-Nahar”, kwa kunukuu vyanzo vyake maalumu, liliripoti kuwa moja ya sababu za kufutwa safari ya Kamanda wa Jeshi la Lebanon, Jenerali Mkuu Rodolph Haykal, kwenda Marekani, ilikuwa ni kupinga kwake kushiriki mkutano uliokuwa umepangwa kufanywa kwa heshima yake, ambao ungejumuisha maafisa kadhaa waandamizi na maafisa wa kijeshi waliounganishwa na balozi, wakiwemo pia maafisa kadhaa wa “Kizayuni”.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kufutwa kwa safari hiyo kulitokea saa chache tu kabla ya muda uliopangwa, baada ya maseneta kadhaa wa Marekani kuanzisha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Kamanda wa Jeshi; hatua ambayo ilionekana kuwa ni ujumbe mkali kwa taasisi ya kijeshi ya Lebanon.

Kuongezeka huku kwa mvutano kulikuja kufuatia tamko lililotolewa na Uongozi wa Jeshi, ambalo lilikuwa na tuhuma ya wazi dhidi ya “Israel” kwa kukiuka mamlaka ya Lebanon, kuvuruga uthabiti na kuzuia uenezi wa jeshi kusini mwa nchi. Tukio la mwisho katika vitendo hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya “An-Nahar”, lilikuwa ni kulengwa msafara wa doria wa “UNIFIL”. Tamko hilo liliibua hasira ya Serikali ya Marekani na duru za Bunge la Congress.

Sambamba na kufutwa kwa safari hiyo, Ubalozi wa Lebanon mjini Washington nao pia ulitangaza kufutwa kwa sherehe ya mapokezi ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa heshima ya Kamanda wa Jeshi.

Kwa mujibu wa taarifa za “An-Nahar”, faili la Lebanon na maendeleo ya hivi karibuni yamewasilishwa moja kwa moja kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, na sasa yapo chini ya uangalizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na kamati zake maalumu. Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na nafasi ya msingi ya Rubio katika kuandika upya sera ya Marekani kuhusu Lebanon, hasa katika suala la misaada ya kijeshi. Kuendelea kwa ushirikiano na Jeshi la Lebanon kutategemea moja kwa moja misimamo itakayochukuliwa na taasisi hiyo baadaye, hususan katika faili la mipaka na suala la silaha.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha